Sifa na kuabudu

John Lema 2010

kunena kwa lugha

VIKWAZO KATIKA KUNENA KWA LUGHA

Kunena kwa lugha ni mojawapo wa bomu lenye nguvu kubwa kwa Shetani, hivyo Shetani hujitahidi kuleta vikwazo vingi ili kwamba wakristo wasilitumie hili bomu kumlipua.  Shetani amekuwa akitumia watumishi wa Mungu wasiokuwa na ufunuo mpana kuhusu kunena kwa lugha, kupotosha wakristo na kuwafanya wakristo wengi wakose baraka hii.  Watumishi wa Mungu mbali mbali wamekuwa wakizuia kunena kwa lugha.  Kuzuia kunena kwa lugha ni kwenda kinyume na neno la Mungu, ni bora kuwafundisha wakristo matumizi ya karama hii ya kunena kwa lugha na kuiruhusu ifanye kazi kanisani.  Mungu anasema, tusizuie kunena kwa lugha, kwa nini wewe unazuia kunena kwa lugha?  Biblia inasema,

 

Kwa ajili ya hayo, ndugu, takeni sana kuhutubu, wala msizuie kunena kwa lugha.  Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu (1 Wakorinto 14:20).

 

Kikwazo kingine katika kunena kwa lugha kinapatikana kutoka kwa Shetani mwenyewe wakati wa maombi ya kunena kwa lugha.  Wakati unanena kwa lugha usiitafsiri ile lugha kwa kuilinganisha na lugha yako ya kiswahili, kingereza, kifaransa, au kiluya, kisukuma, kiganda, kibembe, kikulya, n.k.  Wakristo wengi wanapokuwa katika kunena kwa lugha wanajaribu kutafsiri yale maneno anayoyanena kwa lugha.

 

Lugha zote duniani ukizitafsiri kwa lugha nyingine, hii siyo kutafsiri, niite kulinganisha. Unachukua neno unalilinganisha katika lugha yako au unalifananisha katika lugha yako.  Hivyo lugha nyingi hapa duniani ukizilinganisha maneno ya lugha hii na kuyapeleka kwenye lugha nyingine yanaweza kuwa na maana mbaya sana.  Yanaweza kuwa ni matusi mabaya au maneno ya aibu na mabaya sana.  Hivyo hata lugha anayoitumia  Roho Mtakatifu maneno yake yanaweza yakafanana na maneno mabaya sana katika lugha fulani au katika kabila lako.  Shetani hutumia kitu hiki kuwadanganya wakristo kuwa anayenena siyo Roho Mtakatifu bali ni Shetani.  Hivyo wakristo hao huogopa kuendelea kunena kwa lugha.  Kuna msemo ambao husemwa na baadhi ya wakristo, wasiojua utendaji kazi wa karama hii, msemo huo ni kwamba, Roho Mtakatifu amemwacha…  Huo ni msemo umebuniwa na Shetani kulipotosha kanisa.  Kwa nini Roho Mtakatifu awe na haraka namna hii ya kumwacha mkristo?  Roho Mtakatifu hawezi kumwacha mkristo hata kama huyo mkristo atatenda dhambi.  Roho Mtakatifu ni mvumilivu sana madamu ikiwa mkristo bado hajamkufuru Roho Mtakatifu.  Neno la Mungu linasema,

 

 

Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.  Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea kwa vile haumwamini wala haumtambui; bali ninyi.  Mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu (Yohana 14:16-17).

 

Unaweza kumzimisha Roho Mtakatifu lakini siyo kukuacha.  Mhusika asipoishi maisha matakatifu anaweza kumzimisha Roho Mtakatifu au mhusika asipokuwa mwombaji wa kunena kwa lugha wa muda mrefu pia anaweza kumzimisha Roho Mtakatifu, vinginevyo wewe mtu wa Mungu japokuwa unaweza kukuta maneno anayonena katika Roho Mtakatifu, unapoyatafsiri yanaweza kuonekana ni mabaya kwa lugha yako ya kienyeji, wewe usijali hilo, huyo ni Roho Mtakatifu bado anakuombea hivyo wewe endelea kuomba tu.

 

Mimi kabila langu ni Msukuma wa Mwanza, Tanzania.  Maneno mengi ya kabila la Baganda wa Uganda, ukiyalinganisha na lugha ya Wasukuma ni mabaya sana.  Hata nyimbo zingine za kikristo za Baganda huwezi kuziimba kwa Wasukuma kwa sababu zina baadhi ya maneno kwa Wasukuma ni aibu sana.  

 

Mfano:

 

Neno la Baganda nyo maana yake ni sana.  Waganda wanapozungumza mara nyingi hulitumia sana hasa mahali wanapoonyesha msisitizo, huliongea kwa kulirudia mara kadhaa, yaani Nyo, Nyo, Nyo, Nyooo!  Ikiwa na maana ya Sana, Sana, Sana, Sanaa!  Neno hili kwa Kisukuma ukilifananisha, maana yake ni kiungo cha mwili wa mwanamke cha kike, yaani uke.  Nimetoa mfano wa neno moja tu, lakini kuna maneno mengi sana.  Katika kila kabila mambo yako hivyo hivyo.

 

Shetani asilitumie hili jambo kukudanganya ili uogope kuendelea kunena kwa lugha, badala yake uombe kwa lugha yako ya kawaida.  Shetani hutumia hali hii kuwapotosha wakristo hadi wamekuwa wakifikiri kuwa huenda hawakujazwa Roho Mtakatifu bali huenda walijazwa mapepo.  Mtu wa Mungu kama kweli umeokoka huwezi kujazwa pepo bali unajazwa Roho Mtakatifu.  Hata wakristo wengine wasiojua kwa upana kuhusu kujazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha, wamekuwa wakiwapotosha wakristo na kuwaambia, eti wananena lugha za mapepo. 

 

Mtu wa Mungu huo ni uongo wa Shetani kuwapotosha watu wa Mungu.  Mtu aliyeokoka hawezi kujazwa pepo ni lazima ajazwe Roho Mtakatifu, hata kama utanena kwa lugha na maneno mengine ukiyafananisha katika kabila lako unayakuta kama unatukana watu au unasema matusi, huyo bado ni Roho Mtakatifu wala siyo mapepo.  Neno la Mungu linasema,

 

Ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanaye akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge?  Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je Baba yenu aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao? (Luka 11:13).

 

Baada ya mtu wa Mungu kujazwa Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu huendelea kukaa nawewe hadi utakapofika mbinguni.  Mtu wa Mungu kama hujamkufuru Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu hawezi kukuacha isipokuwa unaweza kumzimisha.  Kumzimisha Roho Mtakatifu ni ile hali ya kwamba, ulikuwa unanena kwa lugha sasa hali hiyo imetoweka, huneni kwa lugha tena.

 

NB:

 

Nitazungumza kwa kifupi kuhusu kukufuru Roho Mtakatifu huko mbele.

 

Biblia inasema,

 

            Msimzimishe Roho Mtakatifu (1 Wathesalonike 5:19).

 

Mtu uliyejazwa Roho Mtakatifu unatakiwa uendelee kuwa unanena kwa lugha na uishi maisha matakatifu, vinginevyo utajikuta kunena kwa lugha kumezimika.  Hapo ndipo utakuwa umemzimisha Roho Mtakatifu.  Baada ya kumzimisha Roho Mtakatifu ili uanze tena kunena kwa lugha kuna hitajika siku hiyo kushuke nguvu kubwa ya Mungu kwa mfano wa mtu yule anayejazwa Roho Mtakatifu kwa upya.

 

Jambo lingine

 

Wakristo wengi katika siku zao za mwanzo baada ya ujazo wa Roho Mtakatifu, hunena kwa lugha kwa mtindo wa kusema sentensi moja na wanaendelea kuirudia sentensi hiyo hiyo moja na kuendelea pengine hadi mwisho wa maombi.  Wengine nao hunena kwa lugha wakisema neno moja tu na wanaendelea kulirudia neno hilo moja pengine hadi mwisho wa maombi.  Wakristo wengi, jambo hili huwachanganya na kuona kuwa huenda katika kuomba vile hawaombei mambo mengi, hivyo wanaamua kuacha kunena kwa lugha, badala yake wanaanza kuomba kwa akili.

 

Wachunguzi wa Biblia wanasema kuwa hapa duniani kuna lugha maelfu, kuna lugha zingine ngeni ambazo hata hazijawa na maneno yote.  Lugha kama Kiswahili ni lugha ngeni hata bado haina maneno mengine.  Watafiti wa Kiswahili bado wanatunga maneno ambayo hayapo.  Kuna lugha zingine za zamani hata zilishakufa, kama lugha ambayo walikuwa wanaiongea wajengaji wa mnara wa Babeli.  Lugha hiyo ilikufa siku hiyo. Wachunguzi wengine wa Biblia wanadhani kuwa huenda ndiyo lugha inayozungumzwa na watoto wadogo na kuna lugha zingine zinayo maneno mengi.  Mfano ni barua iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ukiitafsiri katika lugha ya Kiingereza, barua ya Kiswahili itakuwa ndefu sana, lakini barua ya Kiingereza itakuwa fupi sana.

 

Kuna kabila moja linalopatikana mkoa wa Singida, Tanzania, kabila hilo linaitwa Wasandawi.  Hawa Wasandawi lugha yao wanayoongea utafikiri mtu anapiga busu au anafyonza.  Herufi za maneno yao huwezi kuziandika na ukisikiliza wanaongea huwezi ukatofautisha kati ya neno lililomaliza kuongewa na linalofuatia kusemwa.  Hivyo kuifanya sentensi nzima ionekane kama ni neno moja limeongewa na kurudiwa neno hilo hilo moja mara kadhaa.  Kuna lugha nyingi tu hapa duniani ambazo ukizisikiliza utaona ziko katika mfano huu wa lugha ya Kisandawi.  Ukifungua radio, vituo vya nchi za mbali sana na nchi yako, ukisikiliza utasikia wanaongea neno moja na wanaendelea kulirudia neno hilo hilo, wakati mwingine yanaweza kutofautiana kidogo, lakini utaona sentensi au wanavyoongea utapata kuona wanaongea maneno mawili au matatu.  Hapa siyo wanaongea neno moja na kulirudia hilo hilo au wanaongea maneno mawili au matatu na kuendelea kuyarudia hayo hayo, ila kwa vile wewe huifahamu lugha hiyo, halafu inatofautiana kwa mbali sana na lugha yako, hivyo huwezi kutofautisha neno hadi neno, bali wewe utafikiri neno la kwanza linafanana na lililofuatia, kumbe hayo maneno yanatofauti kubwa.

 

Lugha anayotumia Roho Mtakatifu pengine ukiisikiliza inaweza kufanana na maelezo hayo hapo juu, unapoisikiliza huwa unaona kama unaongea neno moja tu na unaendelea kulirudia hilo hilo pekee toka mwanzo wa maombi pengine hadi mwisho wa maombi.

 

Pengine unaweza ukasikia unaongea sentensi moja na unaendelea kuirudia hiyo hiyo sentensi hadi kiasi kuwa sentensi ya kwanza inafanana na sentensi inayofuatia na inafanana na sentinsi zingine zitakazoendelea.

 

Wakristo wengi kwa kutokufahamu hili huona kuwa huenda hawaombi mambo mengi wanapokuwa wakinena kwa lugha.  Wakristo wakisikia neno moja hilo hilo Roho Mtakatifu anaendelea kulirudia au sentensi hiyo hiyo moja inaendelea kurudiwa rudiwa, baada ya kuona hivyo wakristo wengi huamua kuacha kunena kwa lugha na kuamua kuomba kwa akili zao.  Usiisikilize lugha ya Roho Mtakatifu kwa mtazamo huu, huwezi kuitofautisha wakati mwingine kati ya neno na neno, utafikiri maneno yanayosemwa yanafanana kumbe hayafanani.  Wakristo wengi wakiona hivyo, hufikiri kuwa Roho Mtakatifu haombei vitu vingi.  Hapana, pamoja na hali hiyo Roho Mtakatifu anakuwa anaombea vitu vingi sana.  Hivyo wewe mtu wa Mungu pamoja na kusikia kama anarudia sentensi moja au anarudia neno moja, mtu wa Mungu wewe endelea kunena kwa lugha, usikatishe kunena kwa lugha ukarudi katika maombi ya akili kwa sababu hii.  Hili Shetani amekuwa akilitumia kuwapotosha wakristo ili wasiombe katika Roho Mtakatifu muda mrefu.

 

Biblia inasema, Roho Mtakatifu hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 

 

Kuugua nini?

 

Kuugua ni sawa na hali anayokuwa nayo mama mjamzito, zile dakika tano kabla ya kujifungua mtoto.  Ile hali ya uchungu wa kujifungua, hali kama hiyo ndiyo kuugua.  Kuugua pia kunapatikana kwa watu waliofiwa na watu wa karibu sana.  Watu waliofiwa na mtu wa karibu sana mara nyingi uchungu wanaokuwa nao ndani yao huwa mkubwa sana kiasi huwafanya hata wakose nguvu za kutembea, hubidi watu wa kuwasaidia.  Hali kama hii hasa huonekana kwa wanawake.  Watu wanapokuwa katika kiwango hiki cha uchungu huwa hawawezi hata kulia.  Nguvu za kulia zinakosekana hivyo mtu anaweza kuonekana kama anataka kuzirai.  Wakati mwingine mtu huonekana kama yuko katika maumivu makali sana.

 

Nimekuwa nikiwauliza wanawake mbali mbali waelezee hali ya uchungu wa kuzaa inakuwaje, katika zile dakika tano za mwisho kabla ya kujifungua.  Wanawake wengi wameshindwa kutoa maelezo kwa kudai kuwa hawana lugha ya kuuelezea huo uchungu.  Wanasema ni maumivu makali ambayo hayana mfano wake.  Maumivu yenye kiwango cha juu sana ambacho hakielezeki.

 

Nimejaribu kuwauliza kuwa, pengine maumivu hayo yanaweza kulingana na maumivu ambayo anayasikia mtu aliyepigwa viboko kama arobaini vya nguvu.  Wanawake wote wamekuwa wakijibu ni afadhali kupigwa viboko arobaini kuliko maumivu ya uchungu wa kuzaa.  Nimekuwa nikiwauliza tena kuwa, mtu akipigwa viboko arobaini vya nguvu ni lazima atalia, je, kwa upande wa uchungu huo wa kuzaa huwa inakuwaje kuna kulia pia? Wanawake wengi wamekuwa wakijibu kuwa, Huwezi hata kupata nguvu ya kulia.

 

Hii picha ninajaribu kukuonyesha kuwa maumivu makubwa sana huwezi kulia.  Hivyo kadri maumivu yanavyozidi kuwa makubwa hata nguvu ya kulia haiwezi kupatikana.

 

Kwenye kilio (msiba) hujitokeza watu wa aina tatu.  Aina ya kwanza ni watu wasio na uhusiano kabisa na aliyekufa.  Wao ameenda kwenye kilio kwa vile wako mtaa mmoja au wanafanyakazi mahali pamoja.  Aina ya pili ni watu walio na uhusiano wa mbali kama vile ndugu wa mbali; watu hawa ile hali ya kutokumwona tena mtu waliomzoea inaweza kupelekea wakalia.  Kundi hili huwa pamoja na marafiki.  Aina ya tatu ni watu wale wenye uhusiano wa karibu sana na marehemu, kama vile wazazi, watoto, dada, mume, mke, watu wanaomtegemea katika maisha yao, n.k.  Aina hii ya tatu ya watu wa karibu huwa na uchungu mkubwa sana kiasi kwamba huwa hawawezi hata kulia, hata kutembea huhitaji msaada wa kushikwa huku na huku ili waweze kutembea na wengine huwa hawawezi kutembea kabisa. 

 

Biblia inasema,

 

Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa (Warumi 8:26).

 

 

Nimejaribu kujitahidi ili nieleze angalau kwa sehemu kuhusu jinsi Roho Mtakatifu anavyoweza kutuombea kwa kiwango cha kuugua.  Neno la Mungu linasema kiwango cha kuugua ambacho Roho Mtakatifu anakifikia hakiwezi kuelezeka.  Ni kuugua kwa kiwango cha juu sana ambacho hakiwezi kuelezeka.

 

Mtu wa Mungu unapokuwa unaomba kwa kunena kwa lugha, mruhusu Roho Mtakatifu akuombee kwa kiwango cha juu sana.  Iwapo Roho Mtakatifu atakuongoza kuwa katika hali ya kuugua usijizuie.  Kama Roho Mtakatifu atakuongoza kulia, basi wewe usijizuie  kulia, bali lia tena ikiwezekana lia sana.  Wakristo wengine wanapokuwa wananena kwa lugha, hali ya kulia inapojitokeza wanakuwa hawataki kumruhusu Roho Mtakatifu ili awaongoze kulia, wanafikiri kuwa wakilia hawatakuwa wanaombea vitu vingi.  Sisi ni watoto wa Mungu, kulia mbele za Baba yetu ni muhimu, inaonyesha msisitizo wa kuhitaji msaada juu ya mahitaji yetu tuliyoyaomba mbele za Mungu.  Yesu mwenyewe alikuwa anaomba hadi analia ingawaje alikuwa ni Mtakatifu.

 

Biblia inasema,

 

Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu (Waebrania 5:7).

 

Siku moja nilikuwa ninahubiri kwenye kanisa fulani, wakati wa  maombi ya kila mmoja kuomba kivyake, ambayo niliwataka kila muumini amwombe Mungu.  Mama mmoja alilia sana.  Mchungaji wa kanisa lile alinisogelea na kunieleza kuwa, Huyu mama nimemwambia aache dhambi naye hataki, angalia sasa Roho Mtakatifu anamlilia, tena humlilia kila siku.

 

Mchungaji huyu hakujua mambo ya kuomba katika Roho Mtakatifu jinsi anavyowaombea watu.  Ilinibidi nilifundishe kanisa pamoja na yeye, pia nikamtia moyo huyu mama ambaye alikuwa amevunjwa moyo na Mchungaji wake katika swala hili la kulia wakati wa maombi.

 

Roho Mtakatifu anaweza kukuongoza kuomba zaidi ya kiwango hata hiki cha kulia.  Mruhusu Roho Mtakatifu akuongoze kuomba kufikia kiwango chochote kile.  Kiwango cha zaidi ya kulia ni kiwango cha kuugua kusikoweza kutamkwa.  Naupenda ushuhuda ambao huwa unatolewa na Mtumishi wa Mungu Moses Kulola, anapokuwa kwenye mikutano yake ya hadhara ya neno la Mungu.  Mtumishi huyu alikwenda kuhubiri nchi ya Zaire.  Akamjia mama mmoja mtumishi wa Mungu anaitwa Domitira.  Mama huyu ni mwombaji sana.  Mama huyu alihitaji maombezi kutoka kwa mhubiri huyu.  Kutokana na sifa ya huyu mama ya uombaji wake zilizoenea, mhubiri huyu akajiona kuwa yeye hangestahili kumwombea huyu mama, ila huyu mama ndiye anayestahili kumwombea mhubiri.  Hivyo ikawa kila mmoja anataka aombewe na mwenzake. 

 

Katika ubishani huo baadaye mama Domitila akakubali kumwombea Mhubiri.  Mhubiri akapiga magoti akafunga macho.  Mama Domitila akaweka mikono juu ya kichwa cha mhubiri.  Mhubiri hakusikia mama Domitila akiomba, bali akasikia ukimya.  Wakati huo huo Domitila aliitoa mikono juu ya kichwa cha mhubiri.  Baada ya muda kama wa robo saa, Mhubiri akafikiri kuwa huyu mama kwa vile umetokea ubishani juu ya nani amuombee mwenzake, sasa huenda kutokana na hilo huenda bado mama Domitila naye hajaamua kuomba.  Mhubiri akafungua macho ili amtazame huyu mama, akamkuta huyu mama ameshindwa hata kutamka maneno bali anagugumia tu.  Machozi yameshalowanisha nguo yake kifua chote, ameshindwa hata kuiweka mikono yake juu ya kichwa cha Mhubiri, ameshindwa hata kufunika macho yake na yameshakuwa mekundu huku machozi yakiporomoka.  Mama anaugua katika maombi.

 

Mtu wa Mungu haya ndiyo mojawapo ya maombi ya kuugua.  Roho Mtakatifu hata kama atakuongoza kuomba hadi watu wanapokuangalia washindwe kukutofautisha kati yako na mtu aliyefiwa na mtu wa karibu sana, au na mtu anayesikia uchungu wa kuzaa, wewe endelea kuomba, huyo ni Roho Mtakatifu ameamua maombi yafikie kiwango hicho.  Unaonaje kama wewe ni mchoyo namba moja duniani, aje mtu kwako akakuomba msaada kwa kukubembeleza kwa kuugua kiwango hicho, naamini kuwa utamsaidia shida yake iwapo uwezo wa kufanya hivyo unao.

 

Roho Mtakatifu anamfahamu Mungu.  Hivyo anajua jinsi ya kumuomba.  Anajua kabisa kuwa hitaji lako fulani linahitaji maombi ya kulia au hitaji lako linahitaji maombi ya kuugua.  Mtu wa Mungu hebu lia mbele za Mungu; hebu ugua mbele za Mungu, utauona mkono wa Mungu.  Mungu anasisitiza maombi katika Roho Mtakatifu, ni maombi ya kujijenga imani.  Biblia inasema,

 

Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana na kuomba katika Roho Mtakatifu

(Yuda 1:20).

 

Posted in MAFUNDISHO |

HATUJUI KUOMBA

Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo;  lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa (Warumi 8:26).

 

Kama nilivyotangulia kusema kuwa Roho Mtakatifu anazifanya kazi zake zote kupitia mojawapo wa karama tisa.  Roho Mtakatifu hutuombea kupitia karama ya kunena kwa lugha.  Roho Mtakatifu hutuombea kwa sababu sisi hatujui kuomba.  Wakristo wengine husema wao wanajua kuomba sana, hivyo hawahitaji uombezi kupitia kunena kwa lugha.  Hivyo hawahitaji ujazo wa Roho Mtakatifu wenye kuambatana na ishara ya kunena kwa lugha.   Lakini Mungu anajua sisi hatujui jinsi inavyopaswa, ndiyo maana Mungu akaweka kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu iwe ni kutusaidia kutuombea.  Paulo alijua hili ndiyo maana alikuwa ananena kwa lugha kuliko wengine wote.  Hii ina maana ya kuwa, alikuwa anampa Roho Mtakatifu muda mwingi wa kumwombea.  Hata mimi ninakubali kabisa kuwa sijui kuomba ipasavyo bali ninamhitaji Roho Mtakatifu aniombee, hivyo ninampa muda mrefu wa kutosha ili aniombee.

 

Kwa nini hatujui kuomba?

 

Wanadamu tuna mpaka wa kuelewa mambo yanayotukia hapa duniani, kwa sababu tuko kwenye mwili. Huwezi kuelewa mambo yaliyotokea huko nyuma kabla hujazaliwa; Huwezi kuyaelewa mambo yote yanayotokea hapa duniani kwa wakati huu duniani kote; huwezi kuelewa mambo yatakayotokea wakati ujao; huwezi kuelewa mambo yaliyoko katika ulimwengu wa roho; huwezi ukaelewa mipango ambayo Shetani amekupangia katika ulimwengu wa roho. 

 

Ufahamu wa binadamu una mipaka kutokana na mwili.  Mwili ndiyo unatuwekea mipaka.  Roho Mtakatifu Yeye ni Roho, hana mipaka, anao uwezo wa kujua yaliyopita, yanayotendeka wakati huu duniani kote na yatakayotendeka wakati ujao.  Kutokana na hili wewe ukiomba kwa ufahamu wako kwa akili zako, hutaweza kuombea zile shida za muhimu kulingana na uhitaji wako.

 

Mfano

 

Utakapoombea siku ya kesho, utaombea mambo yaliyo katika ufahamu wako.  Hivyo hutajua mambo mengine mengi ambayo Shetani ameyapanga kukufanyia siku hiyo ya kesho, lakini Roho Mtakatifu anajua mitego yote ambayo Shetani amekutegeshea ili ikupate kesho.  Ukiomba katika Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu ataomba kwa ajili ya mitego hiyo ya Shetani ili Mungu atume Malaika wake ili waitegue mitego hiyo mitego ya Shetani.

 

Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu (Warumi 8:27).

 

Maombi ya Roho Mtakatifu ndiyo maombi ambayo yanampendeza Mungu.  Roho Mtakatifu yeye anamjua Mungu, ametoka kwa Mungu, hivyo anajua ni jinsi gani Mungu anapenda.  Mtu wa Mungu ili maombi yako yawe na uhakika wa mia kwa mia kwamba yamempendeza Mungu basi ni katika kuomba katika Roho Mtakatifu.

 

Katika sehemu ya kwanza ya kitabu hiki inahusu, Msingi wa Maombi.  Nimezungumzia kuhusu milango saba ya maombi.  Kati ya ile milango saba, mlango mmojawapo wa maombi ni Maombi ya Roho Mtakatifu.  Milango mingine ni kuomba kwa imani, kuomba kwa jina la Yesu, kuomba ahadi za Mungu, maombi ya mapatano, maombi ya kufunga na kuomba bila kukoma.

 

Kila aina ya kuomba inatakiwa tuitumie, kwa sababu kuna shida zingine haziwezekani kwenye milango mingine yote, bali inawezekana katika mlango mmoja wapo mmoja.  Hivyo kuna mahitaji mengi sana ambayo hayawezekani kwenye milango mingine isipokuwa kwenye mlango huu wa kuomba katika Roho Mtakatifu pekee.

 

Kwa nini hatujui kuomba?

 

Mtu wa Mungu, hakuna dhambi kubwa wala dhambi ndogo, dhambi ni dhambi, dhambi zote ni sawa.  Wakristo wengi wanapozungumzia dhambi wao hufikiria juu ya dhambi zinazoonekana wazi, zile amri kumi za Mungu.  Yesu alipokuwa anawaosha wanafunzi wake miguu, Petro alikataa kuoshwa.  Yesu akasema kama hutaki kuoshwa miguu na mimi, basi wewe siyo mwezetu.  Petro aliposikia hivyo alisema, Basi kama ni hivyo, basi si miguu tu, nioshe na mwili mzima.  Yesu alijibu, Aliyeoga si wa kurudiwa kuoga, bali kuoshwa vumbi miguu.

 

 Roho Mtakatifu hutuombea hata dhambi ambazo tumezitenda tukasahau kuzitubu.  Hakuna dhambi ndogo wala kubwa, dhambi ni dhambi hata kama itakuwa ndogo.  Mtu akivaa nguo rangi nyeupe safi sana, halafu abebe gunia la mkaa kwenye mabega yake, baada ya dakika tano alitue lile gunia, atajikuta hiyo nguo nyeupe safi siyo safi tena, tena haitamaniki kuvaliwa tena, itakuwa imechafuka haifai tena kuvaliwa hadi ifuliwe.  Huo ni uchafu umeingia mara moja.  Kuna mtu anaweza kuvaa nguo rangi nyeupe safi, akaenda nayo ofisini.  Jioni akirudi nyumbani kutoka ofisini akiingalia ile nguo akaiona bado haijachafuka hivyo akaamua kesho yake aivae tena na kwenda nayo ofisini tena.  Jioni akirudi akiingalia hiyo nguo itakuwa imeanza kuchafuka kidogo, lakini itakuwa bado safi inafaa kuvaliwa tena.  kesho yake anaivaa tena kwenda ofisini.  Jioni akirudi nyumbani nguo hiyo itakuwa chafu haitamaniki tena kuvaliwa.  Hii nguo imechafuliwa na uchafu wa kuingia kidogo kidogo.  Pamoja na uchafu huu kuingia kidogo kidogo lakini mwisho umeichafua kabisa hii nguo sawa na ule uchafu mkubwa wa gunia la mkaa ulioichafua nguo mara moja kwa dakika tano tu.

 

Wakristo wengi wanaona dhambi ni zile kubwa zinazoonekana na watu, dhambi ndogo ndogo hawazijali wala hawazitubu wanapozitenda.  Pamoja na kuokoka kwako hizo dhambi ndogo ndogo ndizo zitakazokupeleka Jehanamu.  Dhambi ndogo ndogo ndizo zinaweka kutu kwenye nyaya za simu ya mawasiliano yako na Mungu.  Ndipo unakuta mtu wa Mungu pamoja na kuomba sana kwake lakini hapati mpenyo wala hapati majibu.  Mawasiliano na Mungu yalishakatika siku nyingi.  Pamoja na hivyo kuna dhambi zingine wakristo wanazitenda huku hawazijui kuwa kutenda hivyo siyo dhambi.

 

Mtu wa Mungu unapokuwa unanena kwa lugha, Roho Mtakatifu anakuombea hata dhambi ambazo wewe hujui kuwa hii ni dhambi lakini unazitenda, Roho Mtakatifu  yupo kwa ajili ya kukuombea hata hizo dhambi.

 

Kuna msemo ambao unapenda kutumiwa na wakristo ambao hawaamini katika kujazwa Roho Mtakatifu  na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.  Kabla ya kuomba hupenda kusema kuwa, Tujitakase.  Mtu wa Mungu kujitakasa ni kugeuka na kuacha njia mbaya.  Sawa, Mungu aliwaambia wana wa Israeli katika mlima wa Sinai kuwa wajitakase siku tatu; lakini tunakuta kwenye agano jipya maandiko yanatuambia kuwa sisi baada ya kumpokea Yesu tunakuwa watakatifu.

 

Watakatifu walioko duniani ndio walio bora.  Hao ndio niliopendezwa nao (Zaburi 16:2).

 

Neno la Mungu halisemi tujitakase bali linasema tuzidi kutakaswa.  Hivyo huwezi kujitakasa mwenyewe bali unatakaswa.  Wakristo wengi msemo huu umewapotosha, hivyo wanakuwa bado wanaendelea kutenda dhambi wakitegemea kujitakasa.  Haya ni mapokeo yanatoka kwenye dini yanayomtaka muunini baada ya kutenda dhambi aende kwenye chumba cha kitubio akatubu dhambi mbele za kasisi, baada ya hapo dhambi zinaondolewa na anapewa malipizi ya kufanya hapo hapo.  Sasa mtindo huu umeingizwa kwenye wokovu na baadhi ya watu wasiojua vizuri neno.  Sasa kwenye wokovu kwa vile hakuna kutubu mbele za viongozi wa dini, bali kwenye wokovu kila mtu anatubu mbele za Mungu, wakristo ambao hawataki kubadili njia zao, hata baada ya kuokoka bado wameng’ang’ania dhambi fulani fulani ambazo wanaendelea kuzitenda, hivyo wanapofikia suala la kumwomba Mungu wanaanza na kujitakasa.  Sisemi kuwa kutubu kabla ya maombi haitakiwi bali toba hiyo haitakusaidia kama huwezi kugeuka na kuiacha dhambi.

 

Hapa mimi sikatai kutubu au sikatai kujitakasa, lakini nataka kukuondoa kwenye wazo la kuendekeza kuwa, hata nikitenda dhambi nitajitakasa au nitatubu.  Wewe mtu wa Mungu kujitakasa kwako kuendane na tendo la kugeuka na kuiacha dhambi hiyo, ndipo kujitakasa kwako kutakuwa na maana.  Kujitakasa au kutubu lakini huku unaendelea kuishi kwenye dhambi hakutakusaidia.

 

Mtu wa Mungu baada ya kuokoka unatakiwa ujifunze neno, hilo neno linatakiwa likubadilishe, uishi sawa na unavyojifunza neno la Mungu.  Siyo kuhusiana na dhambi tu, lakini kuhusiana na maeneo yote ya wokovu, kama kuomba, kushuhudia, kumtolea Mungu, upendo, utakatifu, n.k.  Mtu ukijua neno usipolitenda kwako hiyo ni dhambi.  Hivyo neno la Mungu ndiyo linavyokutakasa.  Basi kama ni neno la Mungu linalokutakasa basi ni Mungu mwenyewe ndiye anayetutakasa.

 

            Mtakatifu na azidi kutakaswa (Ufunuo wa Yohana 22:11).

 

Mtu wa Mungu ujitakase; utubu lakini huku kusikufanye ukavunja uwezo wa kupambana na dhambi ukitegemea kujitakasa, hivyo ukawa huna juhudi katika kujizuia usitende dhambi kwa sababu unatumainia kuwa utajitakasa.

 

Hata hivyo kujitakasa kwa kuomba kwa akili hakutoshelezi.  Makosa tuliyoyafanya bila ya sisi kujua hatuwezi kuyaombea kwa akili maana akili zetu tayari haiyajui.  Kunena kwa lugha ndiyo njia pekee ya kutakaswa.  Unajijenga nafsi.  Mtu anayenena kwa lugha hutakaswa kwa kiwango kikamilifu.

 

Unikumbushe; na tuhojiane; eleza mambo yako upate kupewa haki yao (Isaya 43:26).

 

Biblia inasema, Nikumbusheni mpate kupewa haki zenu.  Mungu amechagua mwenyewe kuwa, sisi tumkumbushe ili tuweze kupewa haki zetu.  Kuna maombi ambayo umeomba miaka mingi iliyopita lakini maombi hayo hadi leo hayajajibiwa.  Pengine umeomba kitu fulani miaka kumi iliyopita, lakini hadi mwaka huu bado hujakipata hicho kitu.

 

Majibu ya Mungu ni ndiyo, hapana au ngoja kidogo.  Pengine Mungu anaweza kukujibu ndiyo au hapana.  Akijibu ndiyo, utakiona ulichokiomba.  Lakini akikujibu, hapana, hutakiona ulichokiomba.  Pengine Mungu amekujibu, Ngoja kidogo.  Jibu la ngoja kidogo pia hukioni kitu ulichokiomba wakati huo huo lakini utakuja ukione baadaye wakati Mungu atakapokupa.

 

Jibu la ngoja kidogo halina maana ya kuwa Mungu amekataa, hapana.  Bali Mungu ameona kuwa akikupa wakati huo pengine hutamudu kukimiliki hicho kitu na wakati huo huo ukaweza kumudu kuendelea kuishi maisha matakatifu.  Hitaji lake Mungu kwako ni wewe uende mbinguni.  Pengine Mungu akikupa hicho ulichoomba kitakufanya ushindwe kuendelea na wokovu, hivyo hicho kitu kukufanya uende Jehanamu.  Pengine umeomba utajiri, sasa Mungu ameona kuwa wakati huu huna nguvu ya kiroho ya kumudu kuumiliki utajiri na ukaendelea na wokovu.  Mungu amekubali kukupa utajiri, lakini hali yako ya sasa kiroho, haiwezi kuumudu utajiri.  Hivyo Mungu anakupa jibu la ngoja kidogo.  Baada ya Mungu kukupa jibu la ngoja kidogo, Mungu huanza kukuandaa kiroho ili kiwango chako cha kiroho kiweze kufikia uwezo wa kuweza kumudu kuumiliki utajiri uliouomba na wakati huo huo bado huo utajiri usiweze kuathiri wokovu wako.

 

Mungu huwatengeneza watu wake, au huwandaa kwa kuwafundisha neno lake, kama neno la Mungu litashindwa kumchonga mtu wa Mungu atengemae kwa kiwango cha kiroho anachokitaka Mungu, Mungu hutumia njia ya kuyaruhusu majaribu makali yampige mhusika ili aweze kukubali kubadilika na kuamua kujitoa nafsi yake zaidi kwa Mungu.

 

Kipindi ambacho Mungu hukitumia kumchonga mtu hadi afikie kiwango cha kiroho kinachotakiwa kinategemea bidii ya mhusika ya kumtafuta Mungu zaidi.  Kipindi hicho kinaweza kuwa wiki, mwezi, miezi, mwaka au miaka n.k.  Sasa tangu mhusika aombe Mungu na akaona kimya hakuna jibu, watu wa Mungu wengi wanakuwa hawajui kama jibu ni hapana au ni ngoja kidogo.  Wengine wanapoona kimya, hakuna jibu, wanafikiri wamepewa jibu la hapana, kumbe jibu walilopewa ni ngoja kidogo.

 

Mungu anapokupa jibu la ngoja kidogo anakutaka usikae kimya bali uendelee kumkumbusha.  Mungu amechagua njia ya sisi tuendelee kumkumbusha, hivyo usipoendelea kumkumbusha Mungu, huwezi kupewa ulichoomba.  Kama kipindi cha ngoja kidogo kitachukua miaka mingi pengine, miaka mitatu, mitano au zaidi, watu wa Mungu wengi huwa hawaendelei kumkumbusha Mungu.  Hivyo husababisha maombi waliyoyaomba wasipewe kabisa majibu yao, japokuwa wakati mwafaka wa kupewa unakuwa umeshafika.  Watu wa Mungu baada ya kuona hawapati waliyoyaomba hukata tamaa, hawaendelei kumkumbusha Mungu.  Lakini Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kumkumbusha Mungu.  Hivyo unapoomba kwa kunena kwa lugha, Roho Mtakatifu anamkumbusha Mungu maombi uliyoyaomba huko nyuma uliyosahau kumkumbusha Mungu.  

 

Mungu anasema,

 

            Ombeni bila kukoma (1 Wathesalonike 5:17).

 

Akawaambia mfano, kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala msikate tamaa  (Luka 18:1).

 

Watu wa Mungu kwa kutokujua neno la Mungu, wengine wanasema unapokuwa umemwomba Mungu kitu, usirudie rudie kukiombea tena;  usiendelee kukiomba tena, bali wewe shukuru tu.  Kuendelea kukiombea ni kuonyesha kuwa huna imani.  Kurudia rudia kukiombea kitu ambacho umeshakiombea isitafsiriwe kama ni upungufu wa imani, bali Mungu ndiye ametuagiza tumkumbushe na tuendelee kuomba bila kukoma.  Kumshukuru Mungu baada ya maombi, hakukuzuii wewe kuendelea kumkumbusha Mungu.  Endelea kumkumbusha Mungu huku ukiendelea kumshukuru pia.

 

Kwa vile Mungu anajua kuwa sisi hatujui kuomba itupasavyo, Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kutuombea.  Hivyo mtu unapokuwa unanena kwa lugha, Roho Mtakatifu hutuombea na humkumbusha Mungu maombi yetu tuliyoyaomba huko nyuma, miaka mingi tuliyokata tamaa kuendelea kumkumbusha.  Roho Mtakatifu humwambia Mungu, Mungu mwaka juzi mtoto wako huyu aliomba nyumba, mwaka huo hukumpa, mwaka jana hukumpa, Mungu mwaka huu Mpe! Mpe! Mpe! unajikuta unapewa kitu ulichokiomba zamani ambacho na ulishasahau, lakini umekipata.  Unashangaa kuwa, Hiki kitu nilikiomba zamani sana hata nilisha sahau, lakini leo nimekipata.  Hicho kitu hukukipata bure bali hiyo ni kazi ya Roho Mtakatifu.  Amekuwa akiifanya wakati unapokuwa unanena kwa lugha.

 

Kwa nini Mungu akumbushwe?

 

Mungu siyo dikteta.  Mungu hawezi kukupa kitu ambacho wewe huna shida nacho, mfano: Mimi nina shida ya nyumba, Mungu akinipa gari wakati mimi sina shida ya gari, bali shida yangu kubwa ni nyumba, nitaliuza hilo gari na kujenga nyumba.  Wewe uliomba utajiri mwaka juzi, Mungu akakujibu ngoja kidogo.  Hivyo mwaka juzi na mwaka jana alikuwa anakuchonga ili kukuwezesha ustahili kupewa utajiri huo.  Sasa mwaka huu uko katika hali nzuri kiroho, kiasi kwamba hata kama utapewa utajiri ule uliouomba mwaka juzi ni sawa, maana utaumudu na pia utamudu kuendelea na wokovu.

 

Lakini tangu uombe utajiri huo mwaka juzi na ukapewa jibu la ngoja kidogo, wewe hukuendelea kumkumbusha Mungu.  Mungu hawezi kukupa utajiri huo mwaka huu japokuwa sasa uko na hali nzuri ya kiroho inayoweza kuumudu utajiri huo bila ya wewe kuanguka dhambini.  Mungu hawezi kukupa kwa sababu mwaka huu hana uhakika wa kwamba hilo hitaji lako bado unalihitaji.  Pengine mwaka huu umeghairi mwenyewe, hutaki tena utajiri.  Hivyo iwapo wewe utakuwa unamkumbusha Mungu, Mungu atajua kuwa kumbe hilo hitaji lako bado unalihitaji hata sasa, hivyo Mungu anakupa.

 

Kuomba kwa ahadi

 

Biblia imejaa ahadi maelfu, ambazo tumeahidiwa tuzipate.  Huwezi kudai ahadi ambayo huijui.  Huwezi kudai haki yako ambayo huijui.  Ahadi ni kupewa kabla hujaomba, watu wengi wa Mungu wako kwenye shida na matatizo mengi.  Shida na matatizo hayo yanawapata wakati haikuwa haki kwao kuwa katika shida na matatizo hayo.  Hii ni kwa sababu hawajui haki zao.  Watu wengi wanajua ahadi chache sana.  Wengine wanajua ahadi hamsini, wengine ahadi mia moja; mia mbili; mia tano; elfu moja, n.k.  Kuna ahadi zaidi ya elfu nane.  Kujua ahadi maelfu siyo kitu kirahisi, kuzikumbuka na kuzidai pia siyo kazi rahisi.  Roho Mtakatifu anazijua na zilizo wakati mwafaka kuzipata ni zipi.    Roho Mtakatifu huzidai ahadi kwa niaba yako na kwa mpangilio unaolingana na uhitaji.  Ukimpa Roho Mtakatifu nafasi ya kukuombea atakuombea hata ahadi usizozijua, hivyo utajikuta unapata baraka hata zile usizoziomba.

 

Roho Mtakatifu ni Wakili

 

Nimefanya utafiti wangu mwenyewe nimegundua kuwa kuna watu wengi sana wamefungwa gerezani wala hawakutenda makosa.  Hata watu wengine wamehukumiwa kunyongwa, lakini hawakutenda kosa.  Hakimu anaposikiliza kesi yeye anakuwa hakuwepo kwenye tukio; isipokuwa wale wanaoshitakiana upande unaodai na upande wa mdaiwa, au upande wa mshitaki na upande wa mshitakiwa, kila upande unatakiwa ujitahidi kumweleza hakimu ili kumshawishi akubaliane na upande huo.  Pamoja na hivyo hakimu huamua kesi kufuatana na vigezo vya sheria vilivyowekwa.  Hivyo wanaoshitakiana ushindi utapatikana kutegemeana na kujua sheria.  Mtu asiyejua sheria atajieleza lakini katika maelezo yake yote yanaweza yakawa bado hayajamsaidia kuviruka vikwazo vya kisheria.  Watu wengi hushindwa kesi hata kama hawana makosa kutokana na kutokujua sheria.  Watu wengi wanapokuwa wana shitaka mahakamani huwabidi kuajiri wakili ili awatetee.

 

Wakili anajua sheria hivyo yeye anaweza kukutetea au yeye anaweza kuelezea maelezo yako mbele ya hakimu vizuri huku akizingatia kuruka vikwazo vya kisheria ambavyo vinaweza kukuangusha.

 

Roho Mtakatifu hutusaidia udhaifu wetu katika kuomba, maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo.  Roho Mtakatifu anamfahamu Mungu vizuri kuliko wewe, Roho Mtakatifu anazifahamu vizuri ofisi za mbinguni, pia anajua kufuatilia maombi yetu katika ofisi za mbinguni anajua yamefikia hatua gani, na anajua kitu gani kinachochelewesha majibu.  Ukimpa Roho Mtakatifu nafasi ya kukuombea utafanikiwa katika maombi yako.

 

Kijana mmoja askari alikuwa amepanga nyumba ya kuishi kwenye mtaa fulani.  Kukatokea ugomvi kati yake na vijana fulani wa mtaa huo huo.  Yule askari akawa anawatishia kuwakamata wale vijana.  Wale vijana wakachoshwa na vitisho vya huyo askari Polisi wakaamua kulipiza kisasi.  Siku moja askari Polisi alitoka kazini saa nane za usiku, alikuwa anakaa peke yake kwenye nyumba hiyo aliyokuwa anaishi.  Wale vijana walijua kuwa siku hiyo angetoka kazini saa nane usiku.  Wakati akiwa kazini wale vijana walichukua nguo za mmoja wao wakaenda kuziingiza ndani ya nyumba ya huyo askari, wakaziingiza kwa mbinu ya hali ya juu.  Askari aliporudi kutoka kazini usiku wa manane amechoka, vijana hao wakapiga mayowe kuashiria kuwa kulikuwa na mwizi amewaibia.  Majirani walikuja kuwasaidia.  Wale vijana wakasema mwizi wamemwona amekimbia.  Wakamtuhumu yule askari Polisi.  Watu wakaenda nyumbani kwa askari Polisi, wakapiga hodi.  Askari akafungua mlango wakamwambia tuna mashaka na wewe kuwa unaweza kuwa umeshiriki wizi uliotokea sasa hivi.  Wakamtaka waingie ndani ili wapekue ile nyumba.  Walipoingia sebuleni wakazikuta nguo zinazodaiwa kuibiwa.

 

Yule askari akakamatwa na akabebeshwa hizo nguo akapelekwa kituo cha Polisi na hatimaye akapelekwa Mahakamani.  Kesi ikaanza.  Wale vijana wakasema tumeibiwa nguo na tumemkamata huyu askari anazo.  Hakimu akawauliza, mnao ushahidi wowote?  Wakasema tunao, Mtaa mzima wanazifahamu hizo nguo kuwa ni zetu na hata fundi aliyezishona yupo.

 

Hakimu akamuuliza askari Polisi.  Hizi nguo ni za nani?  Askari akajibu hizi nguo ni zangu.  Hakimu akauliza, unao ushahidi?  Askari akajibu ninao.  Hizi nguo ni zangu mwenyewe nazifahamu sihitaji mashahidi wa kulithibitisha hili, bali nitalithibitisha mimi mwenyewe.  Ile shati nyeupe vifungo vyake vyote vimeshonewa uzi mweupe.  Kifungo kimoja cha chini kilikatika, sikuwa na uzi mweupe nikakishona kwa  uzi wa khaki.  Ile suruali nyeusi imeshonwa na uzi mweusi, ulifumuka mguu wake wa kushoto sikuwa na uzi mweusi nikaishona na uzi wa khaki pia.  Huyu askari akaendelea kutaja alama mbali mbali kwenye kila nguo hadi akamaliza nguo zote.

 

Kwa kuikata habari hii, mwisho wa yote Hakimu aliamua kuwa, upande wa mashitaka umeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha, bali   upande wa mshitakiwa ametoa ushahidi wa kutosha na Mahakama imeridhika, hivyo mshitakiwa ameshinda kesi na nguo ni mali yake.

 

Watu walishangaa sana waliona kuwa Hakimu amefanya upendeleo kwa askari kwa vile wote ni wafanyakazi wa vyombo vya dora.  Pamoja na kushangaa kwao hawakuwa na la kufanya, ndiyo wameshindwa kesi.

 

Siri ya askari huyo kuishinda hiyo kesi ni kwa sababu alikuwa anajua sheria.  Baada ya askari kuona amekamatwa na mali ya wizi, kwa vile yeye alikuwa anajua sheria alijua kuwa amepatikana na akicheza atafungwa kweli.  Nguo alikuwa anazijua kuwa ni za wale wagonvi wake, hivyo alijua hiyo ni mbinu imesukwa ili yeye afungwe.  Hivyo alipobebeshwa zile nguo hapo hapo yeye alianza kufikiri jinsi ya kujinasua kutoka katika vikwazo vya sheria.  Hivyo alipata mbinu ya kusema, Kuwa hizo nguo ni mali yake.  Hivyo ili likubalike hilo, wakati amebebeshwa hizo nguo alianza kuikariri nguo moja moja jinsi ilivyo.

 

Asingekuwa anajua sheria alikuwa anafungwa.  Mtu wa Mungu umekosa kupata haki zako nyingi, maana hujui kuomba ipasavyo.  Kwa nini ung’ang’nie kujiombea wewe mwenyewe wakati Mungu amekupa msaidizi, wakili wa kukutetea.  Mungu mwenyewe amesema hujui kuomba wewe unajidai kuwa unajua.

Posted in MAFUNDISHO |

KUNENA KWA LUGHA NI NINI?

 

Yesu baada ya kufufuka alipaa mbinguni, kabla ya kufa alikuwa ameahidi kuleta msaidizi Roho Mtakatifu ambaye angekuwa msaidizi wa watu watakaomuamini Yesu.  Siku kumi baada ya Yesu kupaa mbinguni Roho Mtakatifu alishuka.  Biblia inasema,

       

        Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.  Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.  Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, Wakaanza kunena kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka (Matendo ya mitume 2: 1-4).

 

Yesu alipofufuka aliendelea kuwatokea wanafunzi wake kwa muda wa siku arobaini, ndipo akachukuliwa mbinguni.  Tangu kifo chake aliacha wanafunzi mia tano, hadi siku ile Roho Mtakatifu anawashukia walikuwa wamebaki wanafunzi mia na arobaini tu. Hao ndiyo walijazwa Roho Mtakatifu na wakanena kwa lugha mpya.

 

Katika hao ni pamoja na mitume, Mariamu mama mzazi wa Yesu na wengine.  Baada ya hapo  mitume walipokuwa wanahubiri wanafunzi wapya waliwaombea ujazo wa Roho waumini hao wapya.  Tunasoma katika biblia sehemu mbalimbali. Biblia inasema,

 

        Ikawa Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso, akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je, mlimpokea Roho Mtakatifu mlipoamini?  Wakajibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.  Akawauliza, basi mlibatizwa kwa ubatizo gani?  Wakasema, kwa ubatizo wa Yohana.  Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. … Na Paulo alipokwisha kuweka mikono yake juu yao; wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri.  Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili ( Matendo ya mitume 19:1-7).       

       

Na mitume waliokuweko Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria umelikubali neno la Mungu, wakawapeleka Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, … Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu (Matendo ya mitume 8:14-17).

 

Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.  Na wale waliotahiriwa, walioamini, walishangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.   Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha na kumwadhimisha Mungu (Matendo ya mitume 10:44-46).

 

Hii ni baadhi tu ya mistari inayoonyesha kuwa kila aliyekuwa anaamini alijazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.  Bado kuna mistari mingi tu ambayo inayoonyesha ujazo wa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha.  Hivyo watu wa Mungu wameendelea kujazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana tangu wakati huo hadi leo hii.  Mimi mwenyewe nimejazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.  Mimi nimeanza kazi ya Mungu Februari 1983, wote ambao wamekuwa waumini wa Yesu chini ya huduma yangu nimehakikisha kuwa kila mmoja amejazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana. Waumini hao ni wengi ni maelfu ya watu.

 

Ujazo wa Roho Mtakatifu wa aina ya maigizo ambao hakuna ishara ya kunena kwa lugha kutokea, mimi mtumishi wa Mungu Godbless Senga ambaye nimepewa neema ya kulifundisha neno la Mungu kwa usahihi, ili mafundisho haya yalipeleke kanisa la Tanzania katika uamsho mkuu, ninaukataa ujazo wa aina hiyo. Huo siyo ujazo wa Roho Mtakatifu kabisa.  Hayo ni maigizo ambayo hayana hata Mungu ndani yake.  Ni kudanganya watu.  Ujazo huo wa maigizo ni maarufu kwa jina la Kipa imara. Mtu wa Mungu unayekwenda mbinguni hakikisha unajazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa luhga imetokea.  Wapagani wanajazwa mapepo ili wafanikiwe lakini kanisa la Mungu bado wanabishana kuhusu kujazwa  Roho Mtakatifu, kwamba wajazwe au wasijazwe.  Ni lazima ujazwe na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.

 

Ishara ya kunena kwa lugha ni ya muhimu kwa mkristo kwa sababu ni moja ya karama tisa.  Kunena kwa lugha ni ishara ambayo tangu mwanzo wa kanisa la mitume tumeona kila anayejazwa Roho Mtakatifu alinena kwa lugha, hivyo ina umuhimu wa pekee ndani ya mkristo kama titakavyoona katika kitabu hiki.  Pia tunaona katika biblia makuhani na manabii nao walijazwa Roho Mtakatifu na wakanena kwa lugha. 

 

 

 Roho Mtakatifu alikuja kuzisimamia kazi zote za Mungu hapa duniani.  Baada ya kuja kuanzia hapo kazi zote za Mungu zikamilikiwa na Roho Mtakatifu.  Roho Mtakatifu ndiye mtendaji wa kazi zote za Mungu, nje ya Roho Mtakatifu hakuna kazi yoyote ya Mungu inayoweza kufanyika.  Kazi zinazofanywa na Roho Mtakatifu ni nyingi sana, anafundisha, anatuonya, anatuongoza, anafariji, anatutia moyo, anatuombea, anatenda miujiza, anaponya n.k.  Kazi za Roho Mtakatifu anazifanya katika maeneo yote ya maisha ya mkristo.  Roho Mtakatifu ili aweze kazi zote, bila ya eneo lolote la kumhudumia mtu kusahaulika, huzifanya kupitia mpangilio maalumu.  Ili serikali imudu kuwahudumia wananchi wake bila eneo lolote la maisha kusahaulika, serikali imegawa majukumu katika wizara mbalimbali ambazo hutekeleza majukumu hayo.  Maswala yote yanayohusu elimu, yanashughulikiwa kupitia Wizara ya Elimu, maswala ya ulinzi yanashughulikiwa kupitia Wizara ya Ulinzi, kuna Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mali ya Asili, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Nchi za Nje, n.k.  Roho Mtakatifu hufanya kazi zake zote kupita karama tisa, karama ya neno la hekima, karama ya neno la maarifa, karama ya kupambanua roho, karama za kuponya, karama ya miujiza, karama ya imani, karama ya unabii, karama ya aina za lugha na karama ya tafsiri za lugha.    Nje ya karama hizi hakuna kazi ya Mungu inayoweza kufanyika. Utendaji wote wa Roho Mtakatifu hupitia karama hizi tisa.  Kazi zote za Mungu zinazofanyika hapa duniani kwa sasa kila mojawapo anazifanya Roho Mtakatifu, kupitia mojawapo wa karama hizi.  Huduma zote za Roho Mtakatifu;  Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji na Mwalimu, huduma hizi hufanya kazi zake kupitia moja au zaidi kati ya karama hizi.

 

Kunena kwa lugha ni mojawapo kati ya karama tisa.  Ni karama iliyo katika kundi la karama tatu za uvuvio karama hizi ni unabii, kunena kwa lugha na tafsiri za lugha.  Zinaitwa karama za uvuvio kwa sababu utendaji kazi wake hujidhihirisha kwa mtu anayetumiwa kwa kushukiwa na kufunikwa na nguvu maalumu ya Mungu, ambayo hudhibiti uwezo wa kuongea wa mhusika na Roho Mtakatifu hutumia midomo ya mhusika.  Roho Mtakatifu huweka maneno yake na mdomo wa mhusika ndiyo hutumika kuyazungumza hayo maneno.  Maneno hayo yanaweza kuwa katika lugha yoyote atakayoamua Roho Mtakatifu.  Kuna lugha za mbinguni (za malaika) na kuna lugha za wanadamu.  Pamoja na hayo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza kwa kutumia lugha inayoeleweka kwa mhusika.  Mtu anayehusika hujikuta anazungumza maneno ambayo hakuyapanga yeye kwa ufahamu wa akili yake, lakini midomo yake hulazimika kuongea maneno yanayowekwa na Roho Mtakatifu.  Mlolongo wa tukio hili ndiyo huitwa kuvuviwa.  Jina lingine la karama za uvuvio huitwa karama za Semi.

 

Mbali na karama za uvuvio kuna karama za ufunuo ambazo ni karama ya neno la hekima, karama ya neno la maarifa na karama ya kupambanua roho.  Karama zingine zinaitwa karama za nguvu, ambazo ni karama ya miujiza, karama ya imani na karama za kuponya.  Katika kitabu hiki sitaeleza kuhusu karama zingine bali nitazungumzia karama ya kunena kwa lugha peke yake.  Mungu amenipa maono ya kuandika kitabu kinachofundisha karama zilizobaki pia.

 

Baada ya mkristo kujazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana, karama zote tisa huwa ndani ya Roho Mtakatifu ndiye huamua ni karama ipi ndiyo ifanye kazi ndani ya mhusika.  Roho Mtakatifu humgawia mkisto mojawapo ya karama au humgawia karama kadhaa, hivyo wakristo hujikuta huyu ana kamara hii na yule ana karama ile, tofauti na mwingine, mwingine anaweza kuwa na karama ya imani, mwingine karama ya unabii, mwingine pengine karama ya neno la maarifa, n.k.

 

Wakristo wote baada ya kujazwa Roho Mtakatifu, ishara ya kunena kwa lugha huonekana mara baada ya mtu kujazwa Roho Mtakatifu, ndiyo hii inayoitwa karama ya kunena kwa lugha.  Pamoja na Roho Mtakatifu kugawa karama kama apendavyo yeye, huyu anapewa hii na yule anapewa ile, karama ya kunena kwa lugha, Roho Mtakatifu amekuwa akiitoa kwa kila mkristo anayejazwa Roho Mtakatifu.  Hivyo kutokana na  hili kila mkristo anayejazwa Roho Mtakatifu amepewa karama ya kunena kwa lugha, isipokuwa yule ambaye yuko katika kungoja kujazwa Roho Mtakatifu.

 

Kunena kwa lugha ni karama ya muhimu sana kwa mtu wa Mungu hii ndiyo maana Roho Mtakatifu amekuwa akimgawia kila mtu wa Mungu.  Mtu wa Mungu wa rohoni ni lazima uwe na karama hii, au kwa lugha nyingine ni lazima ujazwe Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha ionekane.  Kwa nini kila mkristo aliyeokoka na kujazwa Roho Mtakatifu anapewa karama ya kunena kwa lugha?  Hii inaonyesha jinsi karama ya kunena kwa lugha ilivyo ya muhimu sana katika utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu wa Mungu mmoja mmoja.  Kukosekana kwa karama hii ndani ya mkristo kutazuia baadhi ya kazi za Roho Mtakatifu azifanyazo, kwa mkristo mmoja mmoja katika maeneo fulani fulani ya kiroho.    Hii itasababisha mkristo asipate baadhi ya huduma za muhimu sana za Roho Mtakatifu zilizokusudiwa zifanyike kupitia karama hii.  Huduma hizi za muhimu ndizo zimemfanya Roho Mtakatifu ampe kila mtu wa Mungu hii karama ya kunena kwa lugha.

 

Wakristo wengi wamejazwa Roho Mtakatifu na wakanena kwa lugha, lakini kutokana na kukosekana kwa mafundisho hawajui madhumuni ya wao kunena kwa lugha, na hawajui utendaji kazi wa karama hii ndani yao. Hii imesababisha wakristo kuwa hawana nguvu za kiroho za kupambana na dhambi na majaribu mbalimbali ya Shetani.  Shetani amekuwa akiwaweza wakristo ambao wamejazwa Roho Mtakatifu sambamba na anavyowaweza wakristo ambao hawataki ujazo wa Roho Mtakatifu, na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.  Hii imesababisha kutokuonekana umuhimu wa kujazwa Roho Mtakatifu.

 

Maandiko yanaonyesha jinsi kunena kwa lugha kuliko kwa muhimu sana.  Sura yote ya kumi na nne katika kitabu cha Wakorinto wa kwanza, inazungumzia kunena kwa lugha.  Karama zingine zote katika Biblia zimeelezewa kwa sentensi moja moja au kwa neno moja tu.  Karama hii imeelezwa kwa kirefu katika sura nzima, na kuonyesha jinsi gani ilivyo muhimu hii karama ya kunena kwa lugha.  Unaweza kusoma mwenyewe sura yote ya kumi na nne Wakorinto wa kwanza.  mimi nimechukua baadhi tu, ya mistari ambayo itatusaidia kujifunza somo letu.

 

Maana yeye anenaye kwa lugha hasemi na watu bali husema na Mungu maana hakuna asikiaye lakini anena mambo ya siri katika roho yake (1 Wakorinto 14:2).

 

Mtu anapokuwa ananena kwa lugha huwa anasema mambo ya siri katika roho yake.  Hii ndiyo njia pekee ambayo Roho Mtakatifu huitumia ili mkristo amweleze Mungu mambo ya siri kati yake na Mungu.  Hakuna siri ya watu wawili. Maombi unayoyaomba kwa kutumia lugha yako hayawezi kuwa siri. Shetani anaijua lugha yako, lakini Shetani hawezi kuijua lugha ambayo Roho Mtakatifu anaitumia kukuombea.  Mambo ya siri ni mengi sana kama tutavyoona huko mbele.

 

Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake.  Bali yeye ahutubuye hulijenga kanisa (1Wakorinto 14:4).

 

Hii ndiyo njia pekee ambayo Roho Mtakatifu huitumia ili mkristo aweze kujijenga nafsi yake kiroho.

 

Kuhutubu ni kuhutubia au kuhubiri. Neno kuhutubu katika biblia zingine ina maana ya Kutabiri. Kutabiri ni neno lililotumika tangu zamani za manabii likiwa na maana ya kuhubiri. Maana manabii zamani walikuwa wanahubiri kwa kutabiri.

 

Maandiko hayo tuliyoyaona yametupa maana ya kunena kwa lugha.  Hivyo tumeona kumbe kunena kwa lugha ni kuongea na Mungu.  Kuongea na Mungu ni kuomba.  Roho Mtakatifu hutumia midomo ya mhusika kuzungumza na Mungu kwa niaba ya mhusika.  Hii ndiyo njia ambayo Roho Mtakatifu huitumia ili aweze kuwaombea watu wa Mungu.  Kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuombea na hutuombea kwa njia hii.  Kuna watu ambayo hufikiri kuwa Roho Mtakatifu anaweza kumwombea mtu bila ya mhusika kunena kwa lugha.  Huwezi ukamwabudu Mungu kwa kutumia taratibu za kubuni mwenyewe.  Nimetanguliza kukueleza kuwa Roho Mtakatifu huzifanya kazi zake zote kupitia mojawapo wa karama tisa, kazi ya Roho Mtakatifu mojawapo ni kukuombea.  Roho Mtakatifu huifanya kupitia karama ya kunena kwa lugha nje ya hapo hakuna, huwezi kuombewa na Roho Mtakatifu. Wakristo waliojazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha ikaonekana hata wao pia hawawezi kuombewa na Roho Mtakatifu wakati hawaneni kwa lugha, Roho Mtakatifu huwaombea wakati wakinena kwa lugha tu, pekee.

 

Kutokana na hili wakristo wengi waliojazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana, kunena kwao kwa lugha  kwao kumekuwa hakuna maana yoyote.  Wamejazwa  Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha, lakini kunena kwao kwa lugha bado kumeshindwa kuwafanya wawe ni wakristo walio na nguvu, tofauti na wale wakristo ambao hawajajazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.  Nasema hivi kwa sababu wale wanaonena kwa lugha nao hawaneni kwa lugha ipasavyo.   Kwa sababu hawaneni ipasavyo hivyo wamekosa baraka zipatikanazo katika kunena kwa lugha.  Wamekosa baraka hizo za kunena kwa lugha sawasawa na ambavyo wamekosa wakristo ambao hawajajazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana.

 

Kanisa la Korinto lilikuwa limebarikiwa sana na karama hii.  Hata hivyo hawakujua matumizi, madhumuni na makusudio ya kunena kwa lugha, ndipo Paulo alipowaandikia waraka akiwafundisha.  Kanisa la Korinto lilibarikiwa kwa karama zote tisa zikifanya kazi kanisani, lakini kanisa la leo karama hazionekani kwa sababu ya upeo mdogo wa kulijua neno la Mungu.  Wakristo hawafundishwi kwa undani kuhusiana na karama na jinsi zinavyofanya kazi.  Pia karama zinazuiwa zisifanye kazi kanisani.  Paulo anakataa kuzuia kunena kwa lugha.  Anasena,

 

            Wala msizuie kunena kwa lugha (1 Wakorinto 14:39).

 

Kunena kwa lugha ni kwa muhimu sana kusizuiwe bali waumini wafundishwe jinsi ya kuitumia karama hii ili isilete makwazo bali ilete baraka.

 

            Mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa   

            Utaratibu (1 Wakorinto 14:40).

 

Paulo ilibidi awafundishe Wakorinto.  Baada ya kujazwa Roho Mtakatifu na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana Wakorinto walifurahi sana lakini hawakujua matumizi ya kunena kwa lugha, kutokujua matumizi ya karama hii kulileta makwazo.  Waumini hawakutaka tena waombe kwa akili.  Kila kuomba wao walinena kwa lugha.  Hata mmoja wao alipotakiwa kuomba sala kwa niaba ya wengi, aliomba hiyo sala kwa kunena kwa lugha.

Posted in MAFUNDISHO | Leave a Comment

.


Realtime Clock

Gospel Teachings and One To One Enterviews

WAPO RADIO

                                                                                                                                              Ratiba ya vipindi:

0715 - 0800hrs Patapata

0800 - 0845hrs Yasemavyo Magazeti

0845 - 1000hrs Zilizotufikia

1000 - 1200hrs Meza ya Busara

1200 - 1205hrs Habari kwa Ufupi

1800 - 1830hrs DW Idhaa ya Kiswahili

1830 - 1900hrs Duru za Michezo

1900 - 2000hrs Yaliyotokea

tafuta andiko ndani ya Biblia hapa

Enter a verse or keywords
(John 3:16, love, sword of the spirit)

tafuta katika biblia

Search the BibleBibleGateway.com

videos mpya

1762 views - 0 comments
1414 views - 0 comments
1365 views - 0 comments
2031 views - 0 comments

hali ya hewa

Subscribe To Our Site

mtumie rafiki yako

webs

nyimbo za injili-videos

neno la siku ya leo

jiunge nasi

wageni

..


john lema

shuhuda

 • "Bi Getrude Hamphrey, amekaa ndani ya ndoa kwa miaka saba bila kupata mtoto, ?Nilidharauliwa na watoto wadogo, hata ndugu zangu wa karibu, wengi walinicheka na kuniona sifai, nil..."
  getrude humphrey
  aliyepata mtoto
 • "USHUHUDA WA MAONO YA JEHANAMU UTANGULIZI: Ndugu yangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoanguka duniani, lakini wachache wanaozingatia kwa vile watoaji si wa dini zao au si ..."
  nyisaki chaula
  USHUHUDA WA MAONO YA JEHANAMU

Google Translator

mahubiri

comment box

Facebook Fanpage Box

Recent Prayer Requests

 • maisha yangu

  naomba maombi yenu kuhusu mimi na familia yangu ,mungu atulinde siku zote za maisha yetu,kwani tuko kwenye majaribu mazito
 • kupata watoto

  namomba mungu anisaidie niweze kupata watoto wazuri,wakike na wakime.

,

 

 

 

 

Recent Podcasts

.