Sifa na kuabudu

John Lema 2010

unataka kuolewa na nani?

Wengine wanamtazamo wao, ukiwauliza uko tayari kuolewa na nani, anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani?

Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka uelewe . Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi,umehesabu gharama kwanza? Wengine wakiona mchungaji anavyoshirikiana na mke wake katika huduma wanasema na wao, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mama mchungaji, walipokutana pengine hata wito haukuwepo, na labda walikutana wote wakiwa hawajaokoka. walikuja kuokoka baada ya kuoana!

Mungu amewapa utumishi wakiwa kwenye ndoa tayari, kwa hiyo usitamani ndoa yao, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia.

Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri, hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvurugia.

Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa, utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na  mtumishi, hayo ni maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa furaha.

Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi.  Kama hauko tayari kuchukuliana  na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.

Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia kuomba peke yake na Mungu.  Hata saa nyingine unatamani uombe pamoja naye, lakini  Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza ujumbe.

Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia  kupata mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na unamuuliza sasa  wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua ya kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”!

Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto, ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”!

Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”!

Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanyabiashara.

Mfanyabiashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie kusudi lake.

Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya!

Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu, usimnenee kitu cha namna hiyo.

Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini umepata mtoto na akakua na  akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu huyu”.

Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe.

Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya arusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao!

Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu  haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya!

Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na kwenye pua. Sasa kama ni mtu  mweusi sana  ‘ni hatari sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye  ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana.

Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka!

Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, - haviendi namna  hiyo bwana! Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema!

Sasa akitaka kupaka rangi  hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine juu ya uso wake.

Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo rangi! Hiyo ni kumwonea,  maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi!

Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu! Huyu dada kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana?

Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya  vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha.

uko tayari kuoa au kuolewa lini?

Utasikia mwingine anasema, siku Mungu atakapo nipa mume au mke, hii ni hatari sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.

Kila kitu kilichoko chini ya mbingu kimeratibiwa, kwa lugha nyingine, ni kwamba  kila mwanadamu ana kalenda yake, iko kalenda yako ya kuzaliwa, na ipo kalenda ya  matukio na mipango mbalimbali. Mungu anaijua. Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo, anajua mwisho wa maisha yako wakati wewe unapozaliwa.

Katika mwanzo wa maisha yako, Mungu anakuwa amekwishajua mwisho wako; utakavyokuwa; na kama amekwishajua mwisho wako, maana yake ameshatembea kwenye maisha yako yote toka mwanzo mpaka alipofika mwisho, na alipokamilisha maisha yako akarudi mwanzo ndipo akakuongoza kuzaliwa.

Mungu anapokuacha uzaliwe duniani, hakika ujue kabisa ya kwamba amekwisha tembea na wewe katika maisha yako, amesharatibu mambo yako na yako hatua kwa hatua; kwa mfano, kitu gani utafanya, wapi utasoma, utasoma nini, utaolewa na nani au utaoa nani na itakuwa, lini, maisha yako yatakuwaje, utamtumikiaje, mpaka mwisho wako.  Akiishafika mwisho wa maisha yako anarudi mwanzo, akishafika mwanzo anatangaza mwisho tangu mwanzo; kwa hiyo kuanzia hapo unapozaliwa ujue maisha yako yote yamesharatibiwa!

Ni vizuri ufahamu hii mistari itakusaidia, maana inakujengea msingi mzuri wa maisha hapa. Isaya.46:9-10 inasema, “Kumbukeni mambo ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine, mimi ni Mungu wala hapana aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema, shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote”.

Kwa lugha nyingine anatuambia ya kwamba, ‘wewe unaona kila kitu ni kipya, unapoishi kila siku ni mpya, kila dakika inayokuja ni mpya, Mungu anasema hiyo safari unayopita, mimi nilikwishaipita tayari, nikafika mwisho wa maisha yako ndipo nikakuruhusu uzaliwe. Ulipokuwa unazaliwa nikatangaza mwisho wako tangu wakati unazaliwa.

Sasa mimi ninataka nikuambie kama Mungu anajua, na shauri lake anasema litasimama katika maisha yako, ili mapenzi yake ayatende katika maisha yako, unahitaji kuwa mwangalifu. Kwa sababu kuna mpango na saa ya Mungu ya kuoa au kuolewa, -  ipo!

Mungu anapokuletea mawazo ya kuoa au kuolewa, ni kwa ajili yakuimarisha maisha yako na wito wako na kazi na makusudi, ambayo ameyaweka hapa duniani. Atakuletea mtu atakaye imarisha wito wako, atakuletea mtu atakaye saidiana na wewe, uwe ni mwanamke au uwe ni mwanaume.

Mungu anapo kukutanisha na mtu wa kuoana naye ni kwa ajili ya kuimarisha nguvu zenu ili mtimize kusudi la Mungu. Kwa hiyo lazima anajua kuna saa huyu mvulana anahitaji mke, au huyu msichana anahitaji mume! Lakini watu wengi sana hawalifuatilii hili. unahitaji kufikiri mapema, ili uweke kwenye agenda yako ya maombi ujue kabisa mpango wa Mungu ya kuwa unatakiwa kuoa au kuolewa lini. Ninajua kwa wengi kinakuwa kigumu hicho, maana wengine wametamani kuolewa jana, hawajapata wanaume, wengine wangetaka kuoa leo, lakini bado hawajapata msichana wa kuoa.

Wengine wanatamani kuolewa si kwa sababu mpango wa Mungu umefika wa kuolewa; ila ni kwa sababu wanaona muda wao wa kuolewa umefika, wengine wanaona umri umesogea. Mpango wa Mungu juu ya maisha yako, haubabaishwi na jinsi wewe unavyohesabu miaka,jirani zako wanavyohesabu miaka, ndugu zako wanavyohesabu miaka, au rafiki zako wanavyohesabu miaka.

Mungu anajua alichopanga kwa ajili yako, ana kalenda yako kabisa, na kila alichokichagua Mungu ndicho sahihi.

kuoa au kuolewa kunaweza kukubadilishia imani

Wasomaji wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani (unafahamu ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika kitabu cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu). Biblia inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa hekima ya ajabu, na wasichana wakatoka sehemu mbali mbali duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta hawakutaka kuondoka na wakabaki pale kwake.

Kosa alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa wanakuja na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na miungu yao, anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao. Biblia inatuambia wazi kabisa, ilifika mahali wale wakina mama wakamgeuza moyo wake usiendelee kumpenda Bwana.

Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”

Nimeona vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu kabla hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa  na wafuatilie baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka wameganda kama barafu!  Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe kiroho kwa kiwango hicho - wanaweza wakashindwa kusema. Maana kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu yoyote kwa sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na watu wa kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.

Na ukikaa na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata vijana waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo wanajifanya wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia mbona wewe hujaokoka, na ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze, utakuta baada ya siku chache kupita anajifanya ameokoka, lakini ni yakubabaisha  tu ili akupate. Nimekutana na watu wa namna hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia, na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa nakutafuta wewe, nimekupata basi!

Nimeona! Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho nimeona kwa macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu amenifunulia; kwa hiyo hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko sio mafunuo! Akitaka kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda kuhudumu anaambiwa hakuna; anataka kwenda ‘fellowship’, anaambiwa hakuna; kaa hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula na chai na kwenda kulala!

Na ni kwa sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa akaona jinsi ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa. Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza ikakubadilisha. Ndio maana kuna watu wengine wanaolewa, na wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii sio kitu cha mchezo, ni maamuzi magumu sana kuyafanya.  Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa kwa uangalifu sana.

Lakini pia inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana, lakini fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla ya kuingia kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana, kijana mmoja mlutheri, kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa magumu sana kwao, walipofika masuala ya kujadiliana, juu ya imani zao.  Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji wao wakaingilia kati.

Unajua wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza watoto. Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima hicho kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa. Sio umekwisha olewa ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda huko, - ulikuwa wapi toka mapema ili uliseme hili tatizo? Maana unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala marahisi.

Maana wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo lenyewe sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku mmeoana  sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo maana tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani kivyake; sawa, ninyi mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je?  Labda kama hamna mpango wa kuzaa!

Usiende kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo! Unajua kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua, wakati saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa anawakwepa wale watu waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama Yesu alikuwa anakwepa majaribu mengine kwa nini wewe unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako utalishinda tu, kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi, kwa sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.

Imeandikwa hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza yakayumbisha imani yako.

Maana watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa, ndio kwanza  wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia wapi’, hilo sio swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa! Wewe ulikuwa unajua kabisa mwenzako anasali mahali fulani, na wewe unasali mahali pengine, imefika saa mnataka kufunga ndoa mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani, ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo kuwa hivyo.

ndoa inaweza kuua huduma

Ngoja nikutolee mfano wa kibiblia. Unamkumbuka mtu mmoja aliyeitwa  Samson, alimwoa dada mmoja aliyeitwa Delila, utumishi wake ulinyongewa huko kwenye maisha yao ya ndoa. Ukisoma kile kitabu cha Waamuzi.16:21 kinasema hivi, “Wafilisti wakamkamata wakamng’oa macho, wakateremka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”.

Unajua huyu alikuwa ni mtumishi wa Mungu mzuri kabisa. Lakini hakujua ya kwamba yule mwanamke aliyempenda na akamwoa aishi naye alikuwa ni ‘ajenti’. Hakujua ya kuwa  yule dada alikuwa ni ‘ajenti’ wa adui. Yule dada alikuwa ni ‘ajenti’; kabisa akambembeleza mume wake amweleze siri ya nguvu zake, lakini Samsoni mwenyewe alikuwa anaficha kusema siri ya nguvu zake iko wapi. Lakini yule dada alikuwa na ujuzi wa kubembeleza. Akambembeleza yule baba kiasi ambacho akashindwa kuficha siri yake, na akaisema.

Unajua inapofika kwenye masuala ya ndoa inatakiwa muweze kusaidiana, mtu asitumie udhaifu wako kukuangusha, mtu asitumie udhaifu wako kukuzamisha, mtu asitumie makosa yako kukupeleka jehanamu, inatakiwa ukimpata mwenzako ukiwa na udhaifu akusaidie, ukiwa kwenye dhambi akuombee utoke, unaelekea jehanamu akusaidie kwenda mbinguni, ndivyo inavyotakiwa iwe kwenye ndoa.

Lakini ninakuambia ukimpata mtu, na wewe una maisha yanayoelekea  jehanamu, anakuambia nenda salama, hii ni hatari. Yule dada alikuwa anamfuatilia Samsoni kumnyang’anya kitu kilichokuwa ndani yake cha utumishi alichokuwa amepewa na Mungu, na Samsoni hakujua. Alipofika mahali pa kuisema siri yake alifikiri mke wake  ni mwenzake ambaye anaweza akampa siri yake vizuri bila shida.

Ndio maana kwenye ndoa ambazo watu hawaaminiani vizuri, siri zao hawaambiani. Na ikishafika kwenye ndoa, mnasiri mlizozifichana iko shida, maana yake kuna eneo ambalo usingetaka liingiliwe, unafunga na ufunguo, kasha unatembea na ufunguo mfukoni. Ni eneo umeficha, kwenye ndoa mnatakiwa mfahamiane kila siku, na udhaifu wako, na shida ilioko, na matatizo yaliyoko, kila kitu kiwepo peupe, ili mwenzako atafute namna ya kukusaidia.

Samsoni aliona kitu cha tofauti, lakini alikuwa mke wake, maadui wakaja wakamshika, mke wake anatazama na kushangilia. Badala ya Samsoni kumtumikia Mungu, akaenda akawa anasaga ngano gerezani. Biblia inasema wakamtoboa macho.  Kwa jinsi ya rohoni ningekuambia, wanaondoa macho yako ya rohoni, maono ya Kimungu yanapotea, mtazamo wa Kimungu unapotea, mipango ya Kimungu inapotea.

Ndio maana unakuta mtu ameolewa ameokoka, au ameoa huku ameokoka, akifika ndani ya ndoa maono ya Kimungu yanapotea, na utumishi wake unazama.  Anabaki kusema ‘Bwana asifiwe’, kama bado anaweza akaendelea kusema ‘Bwana asifiwe’, lakini ndani ya moyo amenyonywa kiroho na hakuna kitu.

Sasa labda na ninyi ni mashahidi, wewe angalia vijana ambao wameoa na kuolewa, angalia kama bado wanao moto ule ule wa utumishi, ambao walikuwa nao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Wengine wanabaki  kumsingizia Mungu ya kuwa, amembadilishia huduma, wakati sio Mungu, kumbe ni mume wake amembadilishia huduma, au ni mke wake tu amembadilishia huduma! Maana hakuhesabu gharama ya ndoa kwenye wito wake.

Kwa mfano; Mke wako anakutaka nyumbani, huduma inakutaka kila siku uwepo barabarani, usije ukafikiri ni kitu kirahisi hicho. Utafika mahali lazima uamue, unataka kumpendezesha mke wako au unataka kumpendezesha Mungu.Haya si mambo ambayo ni rahisi kuyaweka vizuri na kuyaanisha bila msaada wa Mungu. Na kama alikuwa anajua anaolewa wapi, kusumbuliwa suala la kusafiri kwako kwenye huduma lisingekuwepo, angekua anakutia moyo na kukuombea, na kukusindikiza siku nyingine. Lakini inapofika anaanza kupata shida, maana yake kuoana kwenu kuna kasoro mahali, na kumekuwa mzigo.

uko tayari kuoa au kuolewa kwa muda gani

Sasa ninakupa siri hapa ikusaidie, Kama umekaribia kuoa au kuolewa, na hujawahi kujiuliza maswali ya namna hii, Labda nikuambie kitu cha namna hii kitakusaidia, kabla sijakupa mistari mingine kwenye biblia, ni hivi: Hakuna sababu ya kuolewa na kijana ambaye atakufa baada mwezi mmoja. Au hakuna sababu ya kuoa msichana atakayekufa muda si mrefu baada ya harusi yenu.

Kwa nini uolewe leo uwe mjane baada ya miezi miwili? Na ukiishaolewa umekwisha badilisha kabisa hali yako na ya  mume wako; akiisha kufa wewe sio msichana tena, utaitwa mjane, hata kama umri wako ni mdogo. Tulienda mahali ulani tukasema tunaomba wajane tuwaombee, tulishangaa kuona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni wasichana. Ungeambiwa wameolewa ungekataa, lakini wamefiwa bado wana umri mdogo.

Sasa mimi ninataka nikuulize swali, kwa nini unataka uolewe, halafu mume wako afe baada ya miezi miwili au unataka uoe mke wako afe baada ya mwezi mmoja, au baada ya mwaka? Hakuna kitu kinachosumbua kama hiki. Ngoja nikueleze hili tena ya kuwa ndoa ya pili sio ndoa ya kwanza. Ndoa ya kwanza ina utofauti wake, na ndoa ya pili ina utofauti wake.

Ikiwa unataka kuishi muda mrefu na mwenzi wako wa ndoa unahitaji;

1. Kuwa mwangalifu kutii ile mistari ilioko kwenye biblia inayozungumzia juu ya muda wa mtu kuishi. Kwa mfano: Waefeso 6:1-3 inasema; “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, upate heri, ukae siku nyingi katika dunia”.

Kwa hiyo angalia uhusiano wako na wazazi wako kama bado wako hai. Lakini pia chunguza uhusiano wa huyo anayetaka kukuoa au anayetaka umuoe, na wazazi wake, kama bado wako hai.

2. Omba Mungu akupe maisha marefu na huyo mwenzako hata kabla hamjaamua kuoana. Ili kama kuna mmoja wenu hataishi muda mrefu – basi Mungu awaarifu na kuwaongoza cha kufanya.

Mwingine anataka aingie kwenye ndoa kwa kubahatisha au kwa majaribio. Maana yake ndani ya nafsi yake anajiweka tayari kuachana na mwenzi wake kama anaona mambo ya ndoa yake hayaendi alivyotarajia. Mtu wa namna hii hataweza kuwa mvumilivu na mwepesi wa kutafuta suluhisho kukitokea tatizo katika ndoa yake.

Uamuzi wa kuoa au kuolewa unamtaka mtu aingie katika ndoa asilimia mia moja. Ikiwa hautakuwa tayari kuingia kwenye ndoa kwa asilimia mia moja – tafadhali usiamue kuoa au kuolewa. Utampotezea tu mwenzako – maana hakuna ndoa isio na matatizo. Lakini pia hakuna tatizo ambalo Mungu hawezi kulitatua. Lakini, je, uko tayari kushirikiana na Mungu katika ndoa kwa kiwango cha asilimia ngapi?.

jua ndoa itaunganisha familia zenu mbili

Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana. Kwa sababu unapooa unaingia kwenye undugu na familia nyingine kabisa tofauti, na sio mahusiano ya kwenu tu wawili.  Ninyi ni kigezo tu cha kuunganisha hizo familia mbili, lakini mkiishaoana hizo familia zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.

Ndio maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio suala la kumtazama kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake ili ujue unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika kwenye masuala ya namna hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.

Unaweza ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu, mimi ninakuambia jasho litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata kijana toka kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi mwenzako juu ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa kuwa unaweza kuoa msichana hata kusonga ugali hajui.

Kuna watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari hawezi kufua nguo zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna mashine za kufulia. Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata mashine ya kufulia hawajawahi kuiona! Unafika pale na unauliza mashine iko wapi, wanakuambia yakufanyia nini, - ya kusagia mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa ndio mashine!

Hujui hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli wala namna ya kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika ndoa unaenda kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule na unashangaa kweli maana hujui hata namna kuwasha taa ya chemli! Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala la kujifunza hivi vitu sio suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani wa kuwasaidia, ni lazima wajue kufanya kazi!

Nilienda kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka kuoa kwenye nyumba ya mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au vibaya wakasema usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye uwanja wa nyumba ya wazazi wake, na wanaangalia ile barabara inayokwenda nyumbani  kwao, na wakiikuta chafu, basi wanajua huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza, wanajua hapa kama tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana ni mchafu!

Ukienda kuoa kwenye familia nyingine utakuta wanasumbuliwa na ugonjwa wa kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza ukapata shida sana. Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au kuolewa unakuingiza kwenye familia nyingine kabisa, na inaunganisha  hiyo familia yao na familia yako; kwa hiyo hayo sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa au kuolewa  unawaingiza watu katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu inaweza ikaleta shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.

msamaha

ILI KUJENGA NDOA IMARA NA MAHUSIANO YA KUDUMU1.USIKAE NA DONGE MOYONI

Kitu kizito kuliko vyote kukibena duniani ni DONGE MOYONI (grudges)

Pia unaweza kuathirika zaidi na kile umeweka moyoni kwani mwenzako anaweza kuwa hajui.

Kuweka vitu moyoni bila kuvitoa au kuzungumza na mwenzi wako huweza kuathiri afya na amani.Kawaida kama una hasira hakikisha unazimaliza mapema na kuelewana na mwenzi wako kabla jua halijazama na kama ni usiku hakikisha unaenda kulala huku umeshalitoa donge lako.


2.FAHAMU KWAMBA HONEYMOON SIYO MAISHA NDOA

Kuna tofauti kubwa kati uchumba, Honeymoon na maisha ya ndoa, uchumba na Honeymoon hupewa moto kemikali ambazo zimo ndani yetu. Hatua ya pili ambayo ni ndoa yenyewe hapa tairi linakutana na barabara ili kuweka wazi uimara na udhaifu. Katika ndoa ni majukumu na kuwajibika na familia iliyoanzishwa, wakati uchumba na Honeymoon ni kuburudishana.


3.KUMTANGULIZA MUNGU KWANZA(MSINGI)
Kumweka Mungu kwanza katika ndoa, huleta furaha ya kweli (joy) faraja na ulinzi. Kumweka Mungu kwanza maana yake mume na mke wanaishi kwa utii na amri za Mungu mwanzilishi wa ndoa wanaomba pamoja na kuwa na mahusiano yanayoongozwa na Mungu. Kwa vipimo vya kibinadamu huwezi kuwa na furaha siku zote kwa safari ndefu kama ya ndoa furaha ya kweli hupatikana kwa kumuweka Mungu namba moja.
4.MFAHAMU MWENZI WAKO NA KUJIFAHAMU WEWE MWENYEWE

Baada ya mapenzi ya Honeymoon kwisha wanandoa huwa na mgodi wa kuanza kuchunguzana na kufahamiana. Wakiwa Honeymoon wanandoa huona kila kitu shwari, wakianza maisha ya ndoa kila mmoja huanza kuona makosa kwa mwenzake hata Kirusiyo hiyo ni nafasi ya wanandoa kufahamiana ni nafasi nzuri ya wanandoa kusifiana, kutumia muda pamoja, kupeana zawadi, kusaidiana kazi ndogo ndogo za nyumbani, kubusiana na kukumbatiana (touch)5.KUWA MSIKILIZAJI MZURI

Binadamu ana asili ya kupenda kuongea zaidi kuliko kusikiliza, kusikiliza kuna maana zaidi kuliko kuongea, wanaume Huongea ili kitu kifanyike na mwanamke Huongea kuchangia wazo na hisia zake. Kuna wakati kila mwanandoa anahitaji kusikilizwa wanaume ni vizuri kuwasikiliza wake zao wanapotoa mawazo yao na hisia zao. Mwanamke huongea maneno 45 elfu kwa siku, na mwanaume 15 elfu, ni nani anahitaji kusikilizwa zaidi?6.KICHEKO-SOCIAL ACTIVITIES

Wanandoa wanahitaji kuwa na kicheko siyo kuwa serious kila wakati kutaniana kusikopitilizwa huongeza furaha katika ndoa pia ni zawadi kutoka kwa Mungu. Wanandoa ni muhimu kuwa na wakati ambapo wanaweza kukaa pamoja na kuwa na kicheko iwe ni kuangalia TV na kusimuliana hadithi ambazo zinawafanya mcheke ni vizuri wanandoa kucheka wakiwa wao wenyewe au wakiwa pamoja na watu wengine. Kicheko huleta raha katika ndoa.7.JIFUNZE KUKUBALI KWAMBA UMEKOSA NA KUOMBA MSAMAHA

Binadamu wote tunafanya makosa na wakati mwingine hayo makosa huumiza tunaowapenda. Lazima tukumbuke wakati tumekosa tunahitaji tuombe msamaha. Usizunguke (indirect way) bali be straight sema “Nisamehe au I am sorry”. Pia usibadili topic au kuanza kusifia ili usiombe msamaha.Pia tunahitaji kufahamu kwamba wenzi wetu si mara zote wapo perfect kama ulivyo wewe (imperfect).

Pia ni vizuri kufahamu kwamba ndoa ni kazi inayoendelea na siyo mwisho wa safari.


8.MHESHIMU, USIMDHARAU

Kumdharau mwenzi wako wakati mwingine huwa kitu rahisi sana. Mwanzo wa mapenzi hata kama kuna hitilafu mara nyingi huitilii maanani, una minimize, lakini baada ya honeymoon kwisha utaona na kukumbuka/ Tambua mambo mengi ambayo huyapendi na unaweza kuanza kupambana nayo na kumdharau mwenzi wako.

Kumdharau mwenzi wako ni kama mmomonyoko ambao ni sumu kwenye mahusiano.

Mwanandoa mwenye busara hawezi kumuaibisha mwenzi wake bali ataongea kwa hekima na kumaliza tofauti zozote kwa upendo.

Kawaida angalia uwezo wake na si udhaifu wake.9.USICHUJE (filtering)

Usimchekeche na kumbandika jina la kudumu kwamba mara zote yupo vile:

Sentensi zinazoanza na haya maneno uwe makini sana
Kila siku unafanya KirusiiKirusii…………………..

Mara zote nakwambia lakini………………

You never……………………

You always……………………

Mara nyingi Ukitokea msuguano wengi huanza kulalama kwa kutumia hayo maneno huwa na maana kwamba unafanya the same mistake over and over na anakupa hicho kibandiko kama jina la mkosaji wa kila siku.

Si kweli kwamba unaweza kufanya makosa yaleyale kila siku, muda wote miaka yote.

10.WEKA MKAZO KWENYE UWEZO NA SI UDHAIFU

Mwanamke na mwanaume wapo tofauti siku zote na ni mpango wa Mungu kuwa tofauti ili kwa tofauti tuweze kusherehekea uumbaji wa Mungu na ili mke na mume waweze kila mmoja kumridhisha mwenzake.

Huwezi kuwa na mwenzi ambaye ana udhaifu mwingi kuliko uwezo na ukiona ana udhaifu mwingi kuliko uwezo basi tatizo ni wewe si yeye.

.


Realtime Clock

Gospel Teachings and One To One Enterviews

WAPO RADIO

                                                                                                                                              Ratiba ya vipindi:

0715 - 0800hrs Patapata

0800 - 0845hrs Yasemavyo Magazeti

0845 - 1000hrs Zilizotufikia

1000 - 1200hrs Meza ya Busara

1200 - 1205hrs Habari kwa Ufupi

1800 - 1830hrs DW Idhaa ya Kiswahili

1830 - 1900hrs Duru za Michezo

1900 - 2000hrs Yaliyotokea

tafuta andiko ndani ya Biblia hapa

Enter a verse or keywords
(John 3:16, love, sword of the spirit)

tafuta katika biblia

Search the BibleBibleGateway.com

videos mpya

1762 views - 0 comments
1414 views - 0 comments
1365 views - 0 comments
2031 views - 0 comments

hali ya hewa

Subscribe To Our Site

mtumie rafiki yako

webs

nyimbo za injili-videos

neno la siku ya leo

jiunge nasi

wageni

..


john lema

shuhuda

 • "Bi Getrude Hamphrey, amekaa ndani ya ndoa kwa miaka saba bila kupata mtoto, ?Nilidharauliwa na watoto wadogo, hata ndugu zangu wa karibu, wengi walinicheka na kuniona sifai, nil..."
  getrude humphrey
  aliyepata mtoto
 • "USHUHUDA WA MAONO YA JEHANAMU UTANGULIZI: Ndugu yangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoanguka duniani, lakini wachache wanaozingatia kwa vile watoaji si wa dini zao au si ..."
  nyisaki chaula
  USHUHUDA WA MAONO YA JEHANAMU

Google Translator

mahubiri

comment box

Facebook Fanpage Box

Recent Prayer Requests

 • maisha yangu

  naomba maombi yenu kuhusu mimi na familia yangu ,mungu atulinde siku zote za maisha yetu,kwani tuko kwenye majaribu mazito
 • kupata watoto

  namomba mungu anisaidie niweze kupata watoto wazuri,wakike na wakime.

,

 

 

 

 

Recent Podcasts

.